Na
Hastin Liumba,Tabora
MKUU
wa mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri ametoa wiki tatu kwa mkurugenzi wa halmashauri
ya manispaa Tabora Sipola Liana kuhakikisha mgogoro wa kiwanja kati ya shirika
la utangazaji Tanzania TBC, halmashauri hiyo na wananchi unapatiwa utatuzi.
Agizo
hilo amelitoa kwenye kikao cha maalumu cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo wakati wa
kuchangia na kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali CAG kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015.
Mkuu
huyo wa mkoa amesema amefuatilia nyaraka za TBC na kugundua kiwanja hicho ni
mali ya shirika hilo, hivyo wananchi wanaoendelea kujenga katika kiwanja hicho ni wavamizi na
waondolewe.
"Natoa
wiki tatu kwako mkurugenzi kuhakikisha mgogoro wa kiwanja cha TBC unamalizwa na
nipewe taarifa kabla ya kuchukua hatua."alisisitiza.
Mwanri
amesema jambo hilo liko wazi lakini anashangazwa na uongozi wa manispaa
kushindwa kuchukua hatua.
"Nilichogundua
kuna udhaifu wa kiuongozi na idara ya ardhi kuna ubabaishaji wa hali ya juu, ni
lazima tuchukue hatua dhidi ya wahusika."ameonya.
Amefafanua
haiwezekani kiwanja kimoja kinatolewa kwa watu wawili na kupelekea mgogoro
baina yao.
Amesema
amepokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wakimueleza Manispaa Tabora
kushindwa kumaliza matatizo hayo.
Amesema
yeye ni mwakilishiwa Rais hivyo asingependa kuona katika mkoa wake watendaji
wanaofanya kazi kwa mazoea na kwamba wanaacha mara moja.
Katika
hatua nyingine baraza la madiwani la manispaa hiyo lilipitisha azimio la kuwasimamisha
kazi watumishi wanne wa idara ya ardhi ili kupisha uchunguzi juu ya tuhuma
mbalimbali zinazoikabili idara hiyo.
Watumishi
hao waliosimamishwa ni Mohammed Matola,Stanley Yungi,Lazaro Iragila na Allan
Mbato ambao wanatuhumiwa na wananchi katika suala zima la viwanja manispaa
Tabora.
Hatua
hiyo ni ya pili kuchukuliwa na baraza hilo la madiwani ambapo kwa mara ya
kwanza iliwasimamisha kazi watumishi watano wa idara hiyo lakini walirejeshwa
kazini mamlaka za juu za serikali.
No comments:
Post a Comment