Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Monday, July 18, 2016

TIZEBA ABAINI MADUDU KWENYE KILIMO CHA TUMBAKU



Na Paul Christian,Tabora.

Waziri wa Kilimo,Mifugo na Uvuvi  Injinia Dkt. Charles Tizeba amefanya ziara ya kikazi mkoani Tabora kwa lengo la kubaini changamoto zinazolikabili zao la tumbaku.

Katika ziara hiyo waziri huyo  ametembelea masoko ya zao yaliyofanyika kwenye vyama vya msingi vya ushirika wa wakulima wa tumbaku vya Tumbi katika manispaa ya Tabora na Ngulu wilayani Sikonge.

Akiwa kwenye masoko hayo ameweza kuzungumza na wakulima,wateuzi (classifiers) , wanunuzi (blenders),viongozi wa vyama vya ushirika, wajumbe wa bodi ya tumbaku Tanzania (TTB).

Akifanya majumuhisho ya ziara hiyo mbele ya wadau wa zao hilo kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Tabora Dkt Tizeba ameagiza yafuatayo:-

·        -Makampuni yanayonunua  tumbaku mkoani Tabora kuwalipa wakulima malipo yao ya pili bila masharti yoyote.

·        -Bodi ya Tumbaku kufanya hesabu ya kilo zilizokuwa zikikatwa na makampuni yanayonunua zao hilo kwa kile kinachodaiwa “mnyauko” ambao unaosababisha uzito wa tumbaku kupungua kwa kuwa mnunuzi amechelewa kuondoa Tumbaku yake kwenye Magodauni baada ya kuinunua, baada ya hesabu hiyo makampuni yatawalipa wakulima kwa msimu huu na misimu mingine iliyopita.

·       - Mabenki yote yaandike mikataba yote kwa lugha ya Kiswahili ili wakulima waweze kuielewa mikataba hiyo.

·        -Mabenki kuacha kuwaibiwa wakulima kwa kucheza na ubadilishaji fedha kutoka dola ya kimarekani kwenda kwenye shilingi ya Tanzania.

·        -Bodi ya Tumbaku Tanzania TTB kuhamisha makao yake makuu kutoka Morogoro hadi mjini Tabora.

·        -Bodi ya Tumbaku Tanzania TTB kuacha kuburuzwa na makampuni yanayonunua Tumbaku au Tobacco Council na badala yake wasimamie sheria kikamilifu.

·        -Bodi ya Tumbaku Tanzania TTB kuanzia msimu ujao wa masoko ifute kabisa matumizi ya mizani ya rula na aina zake zote na badala yake itumike mizani ya electronic ili kuandoa wizi kupitia mizani.

·        -Bodi ya Tumbaku Tanzania TTB ipunguze madaraja ya Tumbaku kutoka 72 ya sasa.

·        -Mabenki kuacha kuyaingiza makampuni ya ununuzi wa Tumbaku kwenye mikataba ya mikopo kwenye vyama vya msingi.

·        -Mrajis wa vyama vya Ushirika nchini kuhakikisha vyama vya msingi ahakikishe vyama vya Ushirika 105 kati ya 217 vilivyoko hatarini kufutwa mkoani Tabora vinarejea kutoa huduma kwa wanachama wao badala ya kuvifuta.

·        -Mrajis atapoteza ajira yake ikibainika chama cha Ushirika au SACCOS imekufa.

·       - Kuanzia msimu ujao Chama Kikuu Cha Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi WETCU LTD hakita endeshwa na fedha ya makato ya moja kwa moja kutoka kwenye kila kilo ya tumbaku na badala yake wataomba fedha kutoka vyama vya msingi ambavyo ni mwanachama wa WETCU LTD na sio mkulima mmoja mmoja.

·       - Halmashauri ya Tumbaku (Tobacco Council) sio chombo cha kisheria hivyo kisitumike kumkandamiza mkulima.

·        -Mkulima hatokatwa kilo moja (mara mbili) kwa ajili ya uzito wa gunia analofungia tumbaku.

·        -Ni mara ya kwanza na ya mwisho kwa mtendaji mkuu wa Bodi ya Tumbaku Tanzania kushindwa kufika kwenye ziara ya waziri mwenye dhamana.

·       - Independent Famers (IF) na Association ni marufuku kwa kuwa zilitumika kuua ushirika.

·        -Wakulima waache kuchanganya grade tofauti za tumbaku kwenye mtumba mmoja.

·        -Wakulima wadhibitiwe kutorosha tumbaku.

·        -Kwenye vyama vya Msingi akopeshwe mkulima mmoja mmoja na sio kwa vikundi ili kila mmoja abebe mzigo wa kulipa deni lake.


Waziri Tizeba amebaini yafuatayo katika ziara hiyo:-

ü -Uchaguzi wa viongozi kwenye vyama vya Ushirika ni Vita kuliko hata kugombea Ubunge.

ü -Tumbaku haijabadilisha maisha ya watu.

ü -Asilimia 90 ya matatizo yaliyoko kwenye vyama vya msingi vya ushirika yamesababishwa na watu walioko nje ya vyama hivyo na asilimia 10 ni wanachama wa vyama hivyo.

ü -Kwenye masoko wanunuzi (Blenders) wanasauti kuliko wateuzi wa serikali (classifiers).

ü -Maofisa ushirika ni chanzo cha kufa kwa vyama vya Ushirika.

ü -Mrajis ni chanzo cha kufa kwa vyama vya ushirika kwa kuwa anaidhinisha mikopo,utoaji fedha,bajeti na nk.

ü -Mabenki ni chanzo cha kufa kwa vyama vya ushirika yanatumia uelewa mdogo wa wakulima kujinufaisha kwa wizi.

ü -Bodi ya Tumbaku Tanzania TTB ni chanzo cha kuua ushirika kwa kuwa imeshindwa kutimiza wajibu wake. 

ü -Tobacco Council inaamua kila kitu na sio Bodi ya Tumbaku Tanzania.
ü Viongozi wa vyama vya msingi wanaingia mikataba wasiyoijua au kuielewa.

ü- Mikopo ya mabenki imekatiwa bima lakini vyama vya msingi vikishindwa kulipa mikopo hiyo bado wanaendelea kudaiwa.

ü -Zabuni za usambazaji Pembejeo zinatolewa kwa misingi ya Rushwa.

ü -Bei ya mbolea inayonunuliwa kwa jumla ni kubwa kuliko bei ya rejareja.

ü- Kwenye soko kuna madaraja 72 ya tumbaku ambapo tumbaku hiyo hiyo ikifika kiwandani Morogoro kuna kitu kinaitwa inhouse grading inayotoa madaraja zaida ya 100.

Sunday, July 17, 2016

TANROADS KUSHIRIKISHA SERIKALI ZA VIJIJI KUBAINI MAENEO KOROFI



Na Paul Christian,Tabora.

Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) mkoa wa Tabora wamepongezwa kwa kutengeneza barabara yenye urefu wa kilometa 46.6 kutoka Ulyankulu hadi Ng’wande ambayo ilikuwa haipitiki wakati wa mvua za masika.

Akiwahutubia wakazi wa vijiji vya Taba,Sasu na Kashishi vilivyopo wilaya ya Kaliua Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu John Peter Kadutu alisema TANROADS mkoa wa Tabora wamefanya kazi nzuri iliyorudisha matumaini ya wakazi hao kuweza kuyafikia maeneo mengine.

Alisema, “Barabara hii ni uti wa mgongo wa mawasiliano ya kiuchumi kati ya wakazi wa jimbo la Ulyankulu upande wa mkoa wa Tabora pamoja na Ushetu na Kahama kwa upande wa mkoa wa Shinyanga.”

Kadutu alifafanua kuwa TANROADS pia wamepanga kuimarisha barabara ya kutoka Makazi kupitia Uyowa hadi makao makuu ya wilaya, Kaliua ambapo hakukuwa na barabara ya uhakika kuunganisha maeneo hayo.

Akizungumzia barabara hiyo mmoja wa wakazi wa kijiji cha Taba Yudita Sayumwa  alishauri, “Wataalam wa TANROADS wanapaswa kuwauliza wenyeji kuhusu maeneo korofi ambayo hukatika wakati wa mvua ili yafanyiwe matengenezo ya uhakika tofauti na ilivyosasa.”

Kaimu afisa mtendaji wa kijiji cha Sasu Samwel Gogoja Ngokolo naye alitoa ushauri kwa meneja wa TANROADS mkoa wa Tabora kuhusisha serikali za vijiji ili kubaini maeneo korofi pamoja na kuweka matuta kudhibiti mwendokasi wa magari eneo la shule ya msingi kijijini humo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Kagera kata ya Kashishi jimboni humo Dennis Steven Mkindo alitaka ufafanuzi kuhusu baadhi ya matengenezo katika barabara hiyo kuonekana dhaifu kwa kuwa haijawekwa molamu.

Akijibu hoja hizo mhandisi wa TANROADS mkoa wa Tabora anayeshughulikia barabara za mkoani humo Siperi Kato alisema, “kazi ya kujenga karavati bado inaendelea na mkandarasi bado hajamaliza kazi.”

Alibainisha kuwa mkandarasi huyo bado anayomakaravati karibu ya 100 na kwamba amekuwa akiyaanda kwa ajili ya kudhibiti maeneo korofi katika barabara hiyo.

Mhandisi Kato aliongeza, “TANROADS kwa kushirikiana na mkandarasi kampuni ya SAMOTA watahusisha viongozi wa serikali za vijiji hivyo ili kubaini maeneo yanayohitaji matengenezo ya ziada kutoka na uzoefu wao.”

Mhandisi huyo alitoa ushauri kwa wakazi wa vijiji hivyo kuzingitia umbali wa hifadhi ya barabara kwa kupima mita 30 kutoka katikati ili kujenga makazi au maeneo ya biashara kwa kuwa imepandishwa hadhi na kuwa ya mkoa tofauti na zamani.

Wednesday, July 13, 2016

WANAWAKE MKOANI TABORA WAHIMIZWA KULIPA KODI



Na Paul Christian, Tabora.

Wanawake wa mkoa wa Tabora wamehimizwa kulipa kodi kupitia shughuli zao za ujasiriamali ili kuisaidia serikali kutekeleza kwa ufanisi miradi ya maendeleo katika maeneo yao.

Rai hiyo imetolewa na mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi UWT mkoa wa Tabora ambaye pia mbunge wa viti maalum Mwanne Mchemba wakati akiwahutubia wajumbe wa Baraza la Umoja huo wa wilaya ya Uyui kwenye kikao kilichofanyika mjini Tabora.

“Na sisi wenyewe kama wanaCCM miongoni mwetu waliokuwepo wasiotaka kulipa kodi uongo, kweli? Sasa mtapataje maendeleo kama hamtaki kulipa kodi.” Alihoji mwenyekiti huyo.

Mwanne amewataka wanawake hao kwenda kwenye maeneo yao kuhimiza wanawake wenzao na jamii kwa ujumla kujenga utamaduni wa kulipa kodi kwa kila shughuli kiuchumi wanazozifanya.

Mwenyekiti huyo wa UWT amesema wanawake hao wanapaswa kudai risiti kila mara wanapofanya manunuzi kwa wafanyabiashara ambao biashara zao ni rasmi na zinatambulika kwa kuwa kwa kufanya hivyo wataiingizia mapato serikali.

Aidha amesema, “kama kuna miradi inakwenda ovyo ni vyema kutoa taarifa kwa diwani wa kata au madiwani wa viti maalum ili wachukue hatua dhidi ya uchakachuaji katika mradi husika.”

Mwanne amebainisha kuwa serikali ya awamu ya Tano imajipambua kwa kupambana na mchwa walikuwa wakiitafuna miradi ya maendeleo kwa wizi na ubadhirifu.

Akitoa salamu kwa  baraza hilo mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM taifa ambaye pia mbunge wa viti maalum mkoa wa Tabora Munde Tambwe amesema wanawake wanapwa kuwa wamoja na kuacha tabia ya kubaguana katika shughuli za kiuchumi.

“Ili kujenga UWT yenye nguvu tunapaswa kuondoa matabaka na hasa baada ya kumalizika kwa uchaguzi ambao ulikuwa na heka heka za hapa na pale na hata kubadilishana maneno.”amesema Munde.

Munde amesema kazi kubwa watakayoifanya wabunge wa viti maalum mkoa wa Tabora ni kuchochea maendeleo kwa wanawake wote pasipo kuwabagua kwa misingi ya itikadi zao.

Amesema, “Sisi ni chama tawala, tufanye kazi ya kuleta maendeleo kwa akinamama wa CCM pamoja na wale wasio kuwa wa CCM, tusiwabague, tusiwatenge katika shughuli za maendeleo, tuwakaribisha tuwasogeze.”

Awali katibu wa CCM mkoa wa Tabora Janat  Kayanda aliwapongeza wanawake hao kwa namna walivyokisaidia Chama Cha Mapinduzi kupata ushindi katika majimbo mawili ya ubunge na kata nyingi wilayani Uyui.
Mwisho.



Saturday, July 9, 2016

VIONGOZI WATANO WA KIJIJI WAPANDISHWA KIZIMBANI KWA TUHUMA ZA UHUJUMU UCHUMIUCHUMI




 Na Thomas Murugwa,Igunga.

Viongozi watano wa  serikali ya kijiji cha Igogo wilaya ya Igunga  mkoani Tabora wamefikishwa mahakama ya Wilaya hiyo wakikabiliwa na mashitaka manne ya kuhujumu uchumi.

Viongozi hao waliopandishwa kizimbani ni mwenyekiti wa kijiji hicho Elinkaila Issa, afisa mtendaji Henry Luhende Masanja, wajumbe wa kamati ya fedha Helena Maduluma  na Boniphace Jagadi pamoja  na mtunza hazina Emanuel Simon.

Upande wa mashitaka ukiongozwa na wakili Edsoni Mapalala wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa  TAKUKURU ulidai mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya Igunga Ajali Milanzi kuwa watuhumiwa walitenda makosa hayo kati ya Oktoba 13 na Novemba 24, 2014.

Katika shitaka la kwanza ilidaiwa kuwa tarehe 13 Oktoba 2014 watuhumiwa kwa kutumia nyadhifa zao waliiba shilingi 5,100,000/- fedha za shule ya msingi Igogo.

Wakili mapalala alisema kuwa watuhumiwa kwa kutumia nyadhifa zao vibaya waliiba kiasi hicho cha fedha ambazo zilikuwa zimetolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa matundu 12 ya vyoo vya shule ya msingi Igogo.

 Ilidaiwa katika shitaka la pili na wakili Mapalala kuwa tarehe 24 Novemba 2014 watuhumiwa kwa pamoja waliiba shilingi 3,120,00/- zilizokuwa  zimetolewa  kwa  ajili  ya ujenzi wa choo cha ofisi ya serikali ya kijiji hicho. 

Katika shitaka la tatu  ilidaiwa na upande wa mashitaka kuwa watuhumiwa kwa pamoja na kwa makusudi  wakiwa  viongozi wa kamati ya fedha ya serikali ya kijiji hicho walijitwalia jumla ya shilingi 8,220,000/- na kusababisha ujenzi wa matundu ya vyoo kutojengwa.

Wakili Mapalala alidai katika shitaka la nne kuwa kutokana na kitendo hicho  watuhumiwa waliisababishia halmashauri ya wilaya ya Igunga hasara ya shilingi 8,220,000/=.

Watuhumiwa wote wamekana mashitaka hayo na wapo nje kwa dhamana hadi julai 12 mwaka huu shauri hilo litakapoanza usikilizwaji wa awali kwani upelelezi wake umekamilika.

Friday, July 1, 2016

MWANRI:AZIGIZA HALMASHAURI KUTENGA ASILIMIA TANO YA MAPATO YA NDANI KWA AJILI YA VIJANA



Na Paul Christian,Tabora

Halmashauri za wilaya na Manispaa mkoani Tabora zimeagizwa kutenga asilimia tano ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuwakopesha vijana katika maeneo yao.

Mkuu wa mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri ametoa agizo hilo jana alipokuwa akifunga mafunzo ya siku tano ya kutambua fursa za ajira kwa vijana 191 wa wilaya ya Uyui yaliyofanyika katika chuo cha kilimo Tumbi katika manispaa ya Tabora.

“Ninaanza kucheck mahesabu ya halmashauri zote za mkoa wa Tabora na nikibaini halmashauri ambayo haijatenga asilimia tano kwa ajili ya vijana hatutapitisha bajeti ya halmashauri husika,” amesema.

Mwanri amesisitiza kuwa suala la kutenga asilimia tano ya mapato ya ndani ya halmashauri hizo ni la kisheria na kwamba halina mjadala.

Aidha amezitaka halmashauri hizo kuweka vipaumbele madhubuti katika mipango yao ili ziweze kuondoa vikwazo vinavyoweza kuwakwamisha vijana kujichukulia fursa mbalimbali za kiuchumi.

“Halmashauri zinapaswa kuweka vipaumbele katika kuchimba mabwawa, kutengeneza miundombinu ya barabara pamoja na mambo mengine kwa lengo la kuwafanya vijana wanaojiajiri wayafikie masoko na kutoa huduma mbalimbali za kibiashara.”Amesema Mwanri.

Mkuu huyo wa mkoa amezitaka halmashauri hizo kutengeneza mazingira wezeshi kwa vijana ili wawe wabunifu wa kujiajiri na kutoa ajira kwa watu wengine.

Akitoa rai kwa vijana hao amesema wanapaswa kubadili mtazamo wa kutaka kuajiriwa na badala yake wafikirie kuwa waajiri wa wale wanaofikiria kuhitimu masomo na kuajiriwa.

Awali kiongozi wa shirika la Millenium Promise Tanzania Dkt. Gerson Nyadzi amesema mafunzo hayo yanatokana na mradi unaojulikana Opportunities for Youth Employment (OYE).

“Vijana hawa wamejifunza nini maana ya mawasiliano,kuwa na nia au malengo katika maisha yao,kuweka kumbukumbu na kuhesabu,namna ya kupunguza msongo (stress management) pamoja na mawasiliano na utambuzi wa fursa.” Amesema.

Amesema mafunzo hayo ni ya awali yanayojulikana kama “stadi za kijamii” na hatua itakayofuata itakuwa ni kufundishwa masuala ya utaalam au ufundi (technical skills training).

Nyadzi amebainisha kuwa katika mafunzo hayo ya awali vijana hao wamejifunza kwa kujigawa katika makundi makuu matatu ikiwemo kilimo cha bustani,ufugaji wa kuku na nyuki.

Ameyataja makundi mengine kuwa ni kutafuta nishati mbadala (renewable energy) ambapo watafanya biogas na utengenezaji wa majiko banifu pamoja na kundi la usafi wa mazingira na maji ( water sanitation and hygiene).

Dkt. Nyadzi amesema vijana hao wenye umri wa kati ya miaka 18 na 30 wanatoka katika kata za Magiri,Ilolangulu,Kigwa,Isila na Isikizya katika wilaya ya Uyui na kwamba walilengwa vijana 210 lakini waliofika na kupata mafunzo hayo ni vijana 191.

Naye mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Uyui Said Ntahondi amemuomba mkuu huyo wa mkoa kuyataka makampuni yanayonunua zao la tumbaku mkoani Tabora kuwatumia vijana hao kupanda miti na shughuli nyingine zinazotokana na zao hilo badala ya kuchukua watu wengine.