Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Wednesday, July 27, 2016

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO



Na Paul Christian, Tabora.

Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu katika kupanga na kutumia rasilimali watu na fedha katika kujiletea maendeleo.

Diwani wa kata ya Cheyo katika manispaa ya Tabora Yusuph Kitumbo ameyasema hayo wakati wa mahojiano maalum kuhusu utekelezaji wa ahadi na ilani ya Chama Cha Mapinduzi katani humo.

Amesema, “kimsingi matumizi bora ya rasilimali watu,fedha na wakati yanategemea mawasiliano madhubuti baina ya viongozi wa ngazi za mitaa na wananchi wanaowaongoza ambapo uibua na kupanga vipaumbele vya maendeleo.”

Kitumbo amesema alianza rasmi kazi ya udiwani mwezi wa Disemba mwaka jana ambapo kazi yake ya kwanza ilikuwa ni kutengeneza daraja la mawasiliano kati ya viongozi na wananchi wa kata hiyo.

Amefafanua kuwa jambo hilo limefanikiwa kwa kuwa katika kipindi cha miezi minane tu ameweza kuongeza watendaji wa mitaa wanne kutoka wawili waliokuwepo kabla ya uchaguzi.

Diwani huyo amesema watendaji hao kwa kushirikiana na wenyeviti wa mitaa wameweza kutengeza mnyororo wa mawasiliano katika kuzikabili kero na changamoto mbalimbali zilizopo kwenye mitaa yao.

Amesema, “kutokana na hali hiyo kata ya cheyo kupitia kamati ya maendeleo  imeweza kuibua mipango ya vipaumbele katika sekta za elimu,afya, miundombinu ya barabara, kusaidia wenye uhitaji watoto yatima na wale wanaoishi kwenye mazingira magumu,wazee na makundi ya ujasiria mali.”

Kitumbo amebainisha kuwa wameweza kutumia fedha zao kuchonga barabara za mitaa ambazo hazikuwepo na kuifanya kata hiyo ambayo ni makazi ya viongozi wa serikali ngazi ya mkoa na wilaya kutofikika kwa urahisi kwenye baadhi ya maeneo.

“Katika kipindi hiki angalau tumetatua kero ya barabara ambazo hazikuwepo na kuifanya kata yangu kufikika kwa urahisi kwa zaidi ya asilimia 50.”Amesema diwani huyo.

Ameongeza kuwa licha ya kuzichonga barabara hizo bado zitakabiliwa na changamoto ya kusombwa au kujaa maji wakati wa mvua hivyo anapigania kupata barabara za lami ili kuwe na uhakika wa kupitika majira yote.

Diwani huyo wa kata ya Cheyo amesema katika suala la kuhakikisha kila mwanafunzi anakaa juu ya dawati, kata yake imeweka rekodi ya kuondoa upungufu wa madawati mapema zaidi kuliko kata nyingine katika manispaa hiyo.

Kitumbo amebainisha kuwa kata ya Cheyo ilikuwa kata pekee kati ya kata 29 ya Manispaa hiyo kupokea madawati 50 kutoka kampuni ya mawasilino ya TIGO jambo lililoondoa upungufu uliokuwepo.

Amesema, “Ingawa kumekuwa na ongezeko kubwa  la wanafunzi wanaoandikishwa katika shule za msingi sita kwenye kata yetu, vyumba vya madarasa vinatosheleza mahitaji.”

Diwani huyo amefafanua kuwa shule hizo za msingi zilikuwa na changamoto ya kugharamia mishahara ya walinzi, ulipaji wa Ankara za maji na umeme ambalo nalo limepatiwa ufumbuzi kwa sasa.

“Kwa sasa shule ya msingi Cheyo A inakabiliwa na changamoto ya madarasa matatu kujaa maji wakati wa mvua kutokana na  ujenzi wa barabara ya kilimatinde,jambo ambalo tunalitafutia ufumbuzi kwa kushirikiana na wahandisi wa Manispaa na TANROADS.”ameongeza Kitumbo.

Kwa upande wa shule ya sekondari ya Cheyo, amesema licha ya kufanya vizuri inakabiliwa na upungufu wa walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati.
Katika kukabiliana na hali hiyo, amesema, “mimi mwenyewe nimejitolea kuwafundisha wanafunzi wa shule hiyo masomo ya Hisabati,Fizikia na Kemia ili nitoe mchango wangu kipindi hiki kigumu.”

Kitumbo amebainisha kuwa katika shule hiyo ya sekondari wamepata mradi wa ujenzi wa vyumba vine vya madarasa na matundu 16 ya vyoo kwa uwiano wa matundu manane kwa ajili ya wavulana na mengine manane kwa ajili ya wasichana.

Aidha amesema mradi huo wa ujenzi utagharimu kiasi cha shilingi milioni 132, fedha ambazo ziko kwenye akaunti ya shule na kwamba ujenzi huo unasimamiwa na Bodi ya shule hiyo.

Kitumbo amesisitiza kuwa fedha hizo zitasimamiwa kwa umakini ili kuhakikisha zinatumika kwa lengo lililokusudiwa na ikibidi zifanye jambo lingine kwa manufaa ya shule hiyo.

Diwani wa kata hiyo ameanisha mipango ya muda wa kati ni kuwasaidia watu wenye mahitaji wakiwemo wazee, wenye ulemavu,watoto yatima na wale wanaoishi kwenye mazingira hatarishi  ili waweze kupata huduma muhimu za kijamii.

Amezitaja  licha ya serikali kutoa elimu bure bado watoto hao wanahitaji chakula,mavazi na malazi ambapo kwa upande wa wazee ni kuhakikisha wanapata huduma za afya bure.

Kwa upande wa Afya amebainisha kuwa katika zahati ya Cheyo ilikuwa ikikabiliwa na upungufu wa watumishi, huduma duni na ukosefu wa dawa pamoja na vifaa tiba.

“Lakini kwa sasa Zahanati ile ni moja kati ya zahanati zinazotoa huduma nzuri za afya, kwa kuwa inawatumishi wa kutosha, dawa zinapatikana pamoja na huduma zimeboreka zaidi.” Amesema.

Akizungumzia malengo mengine ya muda wa kati na mrefu, Kitumbo amesema ni kujenga kituo cha Polisi, Soko na kuipandisha hadhi zahanati iliyopo sasa kuwa kituo cha afya.

Monday, July 25, 2016

WAKAZI WA TABORA WAJIUNGE NA MIFUKO YA BIMA YA AFYA



Na Paul Christian,Tabora.

Wakazi wa mkoa wa Tabora wameaswa kujiunga na mifuko ya bima ya afya ambayo itawasaidia kuwa na uhakika wa matibabu.

Rai hiyo imetolewa na Meneja wa mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF mkoa wa Tabora Vedastus Kalungwani katika mahojiano maalum na waandishi wa habari yaliyofanyika ofisini kwake.

Amesema mifuko ya bima ya afya inamanufaa mbalimbali kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma zinazotolewa kwenye zahanati na vituo vya afya kwa kununua dawa na vifaa tiba.

Kalungwani amebainisha kuwa hadi sasa takwimu zinaonesha kuna mwitikio mdogo wa wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambao unahudumia wakazi wa halmashauri za vijijini pamoja na Tiba kwa Kadi (TIKA) inayohudumia wakazi wa mjini.

Meneja huyo amesema wananchi wanapaswa kutambua umuhimu wa kuwa na bima ya afya kwa kujiunga na mifuko hiyo na kwamba waachane kutibiwa kwa mazoea jambo ambalo linahatarisha uhai wao kwa kuwa magonjwa hayapigi hodi.

Kalungwani amesema Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mkoa wa Tabora umejiwekea mikakati ya kuendelea kuhamasisha wananchi kujiunga na mifuko hiyo kwa kuzifikia halmashauri zote za mkoa wa Tabora.

Meneja huyo wa NHIF mkoa wa Tabora amefafanua kuwa katika mikakati waliojiwekea ni pamoja na kupanua wigo wa huduma kwa kuanzisha mpango wa matibabu kwa wajasiriamali (KIKOA) ambao umelenga vikundi vya waendesha bodaboda, wakulima wa tumbaku pamoja na wajasiriamali wengine kwa kulipia shilingi 76,800/- kwa mwaka ambayo itamuwezesha kutibiwa mahali popote nchini.

Kalungwani amebainisha kuwa katika kuwafikia wajasiriamali hao wamejiwekea lengo la kuvifikia vikundi 990 katika mwaka wa fedha 2016/2017.

Ameongeza kuwa katika kutekeleza mkakati wa mwaka huu wa fedha wameweka mpango wa huduma ya afya kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano unajulikana, “Toto Afya Kadi” kwa gharama ya shilingi 50,400/- kwa mwaka.

Aidha Kalungwani ametaja baadhi ya sababu zinazowakatisha tamaa wananchi kujiunga na mifuko ya bima ya afya kuwa ni pamoja na huduma duni kwenye zahanati na vituo vya afya, idadi ndogo ya wahudumu wa afya,kauli chafu kwa wagonjwa, ukosefu wa dawa na vifaa tiba.

Meneja huyo wa NHIF mkoa wa Tabora ametoa wito kwa wahudumu wa afya kutoa huduma kwa misingi ya viapo vyao vya kazi, maadili ya utumishi na kwa misingi ya weledi wa kitaaluma ili kuwafanya wananchi kuwa na imani ya kupona kwa matibabu wanayotoa.






TANESCO: "FOMU ZA MAOMBI YA KUUNGANISHIWA HUDUMA YA UMEME HAZIUZWI"



Na Paul Christian,Tabora.

Shirika la ugavi wa umeme TANESCO mkoa wa Tabora limesema fomu za maombi ya kuunganishiwa huduma ya umeme kwa wananchi zinatolewa bure kwenye ofisi za shirika hilo ngazi ya wilaya na makao makuu ya mkoa.

Kaimu meneja wa shirika hilo mkoa wa Tabora injinia Melkiad Msigwa ametoa kauli hiyo kufuatia malalamiko ya wakazi wa tarafa ya Ulyankulu wilaya ya Kaliua kudai kutozwa kati ya shilingi 30,000/- na 50,000/- na watu wanajiita mafundi wa umeme ili kupata fomu hizo.

Malalamiko hayo ya wananchi yametolewa hivi karibuni wakati wa ziara ya mbunge wa jimbo la Ulyankulu John Peter Kadutu alipofanya ziara ya kikazi kukagua utekelezaji ya mradi wa usambazaji umeme vijijini ambapo alizungumza na wananchi katika vijiji vya Ibambo,Usigala, Makonge,Mkindo,Kaswa, Taba,Sasu na Kashishi jimboni humo.

Akijibu malalamiko hayo ya wananchi Kaimu meneja huyo wa TANESCO amebainisha kuwa fomu hizo hazipaswi kuuzwa zinatolewa bure na kwamba akitokea mtu anafanya ushawishi wa udanganyifu ili ajipatie fedha akamatwe na achukuliwe hatua za kisheria.

Injia Msigwa amewataka wananchi walioko kwenye vijiji vilivyounganishwa na mtandao wa umeme kupitia mradi wa Usambaji umeme vijijini REA awamu ya pili kuzitumia ofisi za TANESCO kwenye wilaya au kufika makao ya mkoa ya shirika mjini Tabora ili kupata fomu hizo pamoja na taarifa nyingine muhimu.

Aidha amewataka wananchi hao kuwatumia wataalamu kutoka kwenye makampuni yaliyosajiliwa na ambayo yanatambuliwa na TANESCO katika kufanya utandazaji wa miundombinu ya umeme kwenye nyumba na maeneo ya biashara.

Injia Msigwa ametoa onyo kwa watu wanaotumia fursa ya umeme vijijini kujinufaisha kwa udanganyifu kwa kufanya kazi za umeme majumbani pasipo vibali vya serikali kwamba watachuliwa hatua.

Kaimu meneja huyo wa TANESCO mkoa wa Tabora amewataka wananchi, viongozi wa serikali za vijiji na kata ambazo zimepitiwa na umeme kuchukua tahadhari kwa kufika ofisi za TANESCO kupata orodha ya makampuni ambayo yanatambuliwa kisheria, na hivyo kuwa na sifa ya kuwahudumia watu vijijini.


Monday, July 18, 2016

TIZEBA ABAINI MADUDU KWENYE KILIMO CHA TUMBAKU



Na Paul Christian,Tabora.

Waziri wa Kilimo,Mifugo na Uvuvi  Injinia Dkt. Charles Tizeba amefanya ziara ya kikazi mkoani Tabora kwa lengo la kubaini changamoto zinazolikabili zao la tumbaku.

Katika ziara hiyo waziri huyo  ametembelea masoko ya zao yaliyofanyika kwenye vyama vya msingi vya ushirika wa wakulima wa tumbaku vya Tumbi katika manispaa ya Tabora na Ngulu wilayani Sikonge.

Akiwa kwenye masoko hayo ameweza kuzungumza na wakulima,wateuzi (classifiers) , wanunuzi (blenders),viongozi wa vyama vya ushirika, wajumbe wa bodi ya tumbaku Tanzania (TTB).

Akifanya majumuhisho ya ziara hiyo mbele ya wadau wa zao hilo kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Tabora Dkt Tizeba ameagiza yafuatayo:-

·        -Makampuni yanayonunua  tumbaku mkoani Tabora kuwalipa wakulima malipo yao ya pili bila masharti yoyote.

·        -Bodi ya Tumbaku kufanya hesabu ya kilo zilizokuwa zikikatwa na makampuni yanayonunua zao hilo kwa kile kinachodaiwa “mnyauko” ambao unaosababisha uzito wa tumbaku kupungua kwa kuwa mnunuzi amechelewa kuondoa Tumbaku yake kwenye Magodauni baada ya kuinunua, baada ya hesabu hiyo makampuni yatawalipa wakulima kwa msimu huu na misimu mingine iliyopita.

·       - Mabenki yote yaandike mikataba yote kwa lugha ya Kiswahili ili wakulima waweze kuielewa mikataba hiyo.

·        -Mabenki kuacha kuwaibiwa wakulima kwa kucheza na ubadilishaji fedha kutoka dola ya kimarekani kwenda kwenye shilingi ya Tanzania.

·        -Bodi ya Tumbaku Tanzania TTB kuhamisha makao yake makuu kutoka Morogoro hadi mjini Tabora.

·        -Bodi ya Tumbaku Tanzania TTB kuacha kuburuzwa na makampuni yanayonunua Tumbaku au Tobacco Council na badala yake wasimamie sheria kikamilifu.

·        -Bodi ya Tumbaku Tanzania TTB kuanzia msimu ujao wa masoko ifute kabisa matumizi ya mizani ya rula na aina zake zote na badala yake itumike mizani ya electronic ili kuandoa wizi kupitia mizani.

·        -Bodi ya Tumbaku Tanzania TTB ipunguze madaraja ya Tumbaku kutoka 72 ya sasa.

·        -Mabenki kuacha kuyaingiza makampuni ya ununuzi wa Tumbaku kwenye mikataba ya mikopo kwenye vyama vya msingi.

·        -Mrajis wa vyama vya Ushirika nchini kuhakikisha vyama vya msingi ahakikishe vyama vya Ushirika 105 kati ya 217 vilivyoko hatarini kufutwa mkoani Tabora vinarejea kutoa huduma kwa wanachama wao badala ya kuvifuta.

·        -Mrajis atapoteza ajira yake ikibainika chama cha Ushirika au SACCOS imekufa.

·       - Kuanzia msimu ujao Chama Kikuu Cha Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi WETCU LTD hakita endeshwa na fedha ya makato ya moja kwa moja kutoka kwenye kila kilo ya tumbaku na badala yake wataomba fedha kutoka vyama vya msingi ambavyo ni mwanachama wa WETCU LTD na sio mkulima mmoja mmoja.

·       - Halmashauri ya Tumbaku (Tobacco Council) sio chombo cha kisheria hivyo kisitumike kumkandamiza mkulima.

·        -Mkulima hatokatwa kilo moja (mara mbili) kwa ajili ya uzito wa gunia analofungia tumbaku.

·        -Ni mara ya kwanza na ya mwisho kwa mtendaji mkuu wa Bodi ya Tumbaku Tanzania kushindwa kufika kwenye ziara ya waziri mwenye dhamana.

·       - Independent Famers (IF) na Association ni marufuku kwa kuwa zilitumika kuua ushirika.

·        -Wakulima waache kuchanganya grade tofauti za tumbaku kwenye mtumba mmoja.

·        -Wakulima wadhibitiwe kutorosha tumbaku.

·        -Kwenye vyama vya Msingi akopeshwe mkulima mmoja mmoja na sio kwa vikundi ili kila mmoja abebe mzigo wa kulipa deni lake.


Waziri Tizeba amebaini yafuatayo katika ziara hiyo:-

ü -Uchaguzi wa viongozi kwenye vyama vya Ushirika ni Vita kuliko hata kugombea Ubunge.

ü -Tumbaku haijabadilisha maisha ya watu.

ü -Asilimia 90 ya matatizo yaliyoko kwenye vyama vya msingi vya ushirika yamesababishwa na watu walioko nje ya vyama hivyo na asilimia 10 ni wanachama wa vyama hivyo.

ü -Kwenye masoko wanunuzi (Blenders) wanasauti kuliko wateuzi wa serikali (classifiers).

ü -Maofisa ushirika ni chanzo cha kufa kwa vyama vya Ushirika.

ü -Mrajis ni chanzo cha kufa kwa vyama vya ushirika kwa kuwa anaidhinisha mikopo,utoaji fedha,bajeti na nk.

ü -Mabenki ni chanzo cha kufa kwa vyama vya ushirika yanatumia uelewa mdogo wa wakulima kujinufaisha kwa wizi.

ü -Bodi ya Tumbaku Tanzania TTB ni chanzo cha kuua ushirika kwa kuwa imeshindwa kutimiza wajibu wake. 

ü -Tobacco Council inaamua kila kitu na sio Bodi ya Tumbaku Tanzania.
ü Viongozi wa vyama vya msingi wanaingia mikataba wasiyoijua au kuielewa.

ü- Mikopo ya mabenki imekatiwa bima lakini vyama vya msingi vikishindwa kulipa mikopo hiyo bado wanaendelea kudaiwa.

ü -Zabuni za usambazaji Pembejeo zinatolewa kwa misingi ya Rushwa.

ü -Bei ya mbolea inayonunuliwa kwa jumla ni kubwa kuliko bei ya rejareja.

ü- Kwenye soko kuna madaraja 72 ya tumbaku ambapo tumbaku hiyo hiyo ikifika kiwandani Morogoro kuna kitu kinaitwa inhouse grading inayotoa madaraja zaida ya 100.