Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Saturday, June 4, 2016

MSTAAFU ALIA NA HALMASHAURI YA MANISPAA YA TABORA KUSHINDWA KUMLIPA MAPUNJO YAKE



Na Mwandishi Wetu,Tabora

MSTAAFU aliyekuwa mtumishi wa halmashauri ya Manispaa Tabora Daud
Timotheo (70) amelia na uongozi halmashauri hiyo kushindwa kumlipa
haki yake kama mapunjo ya mshahara kiasi cha shilingi milioni 1.3.

Akiongea na waandishi wa habari mstaafu huyo amesema amefuatilia madai yake kwa muda mrefu bila mafanikio hali ambayo imemlazimu kueleza kilio chake hadharani ili asaidiwe kupata haki yake.

Timotheo amesema alistaafu  mwaka 2013 akiwa mhudumu idara ya afya katika halmashauri ya manispaa hiyo na kwamba amepunjwa muda wa miezi 15 kwa kulipwa mshahara pungufu.

Amebainisha kuwa hadi anastaafu mapunjo ya mshahara wake yalikuwa ni jumla ya shilingi milioni 1,392,710.00.

Anasema alikuwa analipwa mshahara wake kwa mwezi shilingi 255,050 kuanzia mwezi Januari 2009 hadi mwezi Novemba 2009.

Aidha ameongeza kuwa katika kipindi hicho  alikuwa akipokea mshahara wa shilingi  128,410.00 ukiwa ni pungufu ya mshahara halisi wa  shilingi 255,050.00

Timotheo amebainisha kuwa hata hivyo alirekebishiwa mshahara wake ambapo mwezi Disemba 2009 alianza kulipwa mshahara wake kamili wa shilingi 255,050.00 lakini mapunjo yake hadi leo hajalipwa na mwajiri wake huyo.

Amesema amechoshwa na hali hiyo ya kuzungushwa kulipwa fedha zake za mapunjo kwa kuwa inamkwamisha kufanya shughuli nyingine ya kujiongezea kipato.

Timotheo anasema amendika barua ya kulalamika ya mwezi Machi 27,mwaka 2010 na kuambatanisha vielelezo vyote (Salary Slip) ya miezi Disemba 2008,Januari 2009 na Disemba 2009.

Mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa ya Tabora Sipola Liana akizungumzia suala hilo amesema kuwa amemuagiza mkaguzi wa ndani kuhakiki deni hilo na taratibu ziandaliwe ili haki ya mstaafu huyo zipatikane.



MWANRI: AAGIZA MGOGORO WA KIWANJA CHA TBC UMALIZWE NDANI YA WIKI TATU



Na Hastin Liumba,Tabora

MKUU wa mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri ametoa wiki tatu kwa mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa Tabora Sipola Liana kuhakikisha mgogoro wa kiwanja kati ya shirika la utangazaji Tanzania TBC, halmashauri hiyo na wananchi unapatiwa utatuzi.

Agizo hilo amelitoa kwenye kikao cha maalumu cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo wakati wa kuchangia na kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali CAG kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015.

Mkuu huyo wa mkoa amesema amefuatilia nyaraka za TBC na kugundua kiwanja hicho ni mali ya shirika hilo, hivyo wananchi wanaoendelea kujenga katika kiwanja hicho ni wavamizi na waondolewe.

"Natoa wiki tatu kwako mkurugenzi kuhakikisha mgogoro wa kiwanja cha TBC unamalizwa na nipewe taarifa kabla ya kuchukua hatua."alisisitiza.

Mwanri amesema jambo hilo liko wazi lakini anashangazwa na uongozi wa manispaa kushindwa kuchukua hatua.

"Nilichogundua kuna udhaifu wa kiuongozi na idara ya ardhi kuna ubabaishaji wa hali ya juu, ni lazima tuchukue hatua dhidi ya wahusika."ameonya.

Amefafanua haiwezekani kiwanja kimoja kinatolewa kwa watu wawili na kupelekea mgogoro baina yao.

Amesema amepokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wakimueleza Manispaa Tabora kushindwa kumaliza matatizo hayo.

Amesema yeye ni mwakilishiwa Rais hivyo asingependa kuona katika mkoa wake watendaji wanaofanya kazi kwa mazoea na kwamba wanaacha mara moja.

Katika hatua nyingine baraza la madiwani la manispaa hiyo lilipitisha azimio la kuwasimamisha kazi watumishi wanne wa idara ya ardhi ili kupisha uchunguzi juu ya tuhuma mbalimbali zinazoikabili idara hiyo.

Watumishi hao waliosimamishwa ni Mohammed Matola,Stanley Yungi,Lazaro Iragila na Allan Mbato ambao wanatuhumiwa na wananchi katika suala zima la viwanja manispaa Tabora.

Hatua hiyo ni ya pili kuchukuliwa na baraza hilo la madiwani ambapo kwa mara ya kwanza iliwasimamisha kazi watumishi watano wa idara hiyo lakini walirejeshwa kazini mamlaka za juu za serikali.

SARATANI YA NGOZI TISHIO KWA MAISHA YA ALBINO.



Na,Thomas Murugwa, Tabora.

Serikali ya awamu ya Tano imetakiwa za kunusuru maisha ya watu wenye ulemavu wa ngozi vinavyotokana na ugonjwa wa saratani ya ngozi.
 
Uchunguzi uliofanywa na blog hii umebaini kuwa vifo 10 vya watu wenye ulemavu wa ngozi  vimetokea kati ya Januari na Mei 2016  mkoani Tabora kutokana na ugonjwa huo kwa kukosa mafuta maalumu  yanayosaidia kupunguza mionzi ya jua kuifikia ngozi ya watu hao.

Katibu wa chama cha Maalbino mkoani Tabora Ramadhani Nassoro amesema  saratani ya ngozi imesababisha vifo hivyo na hiyo imekuwa ni  changamoto kwao kwa kuwa  inachangia kufupisha maisha ya watu wenye ulemavu wa ngozi.

Amesema kuwa watu wanye ulemavu wa ngozi wengi wao maisha yao hayazidi miaka (40) kwa kuwa wanakabiliwa na hatari ya saratani ya ngozi ambayo inatokana na kufikiwa na mionzi ya jua moja kwa moja.

Nassoro amebainisha kuwa albino wanakutana na mionzi ya jua kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kufanya kazi za kujipatia kipato kama kilimo, uchungaji,ujenzi na nyingine katika maeneo ya wazi.

Naye Juma Mosha katibu wa chama cha Albino wilaya ya Nzega mkoani Tabora ameiomba serikali ichukue jukumu la kuwapatia mafuta hayo maalumu kupitia  hospitali na vituo vya afya ili kuwanusuru na saratani ya ngozi ambayo inakatisha maisha yao kwa kiwango kikubwa.

Katibu huyo amebainisha kuwa mafuta hayo yanagharama kubwa hali ambayo albino wengi hawawezi kumudu na kwamba wakati umefika kwa serikali kuwasaidia kama ambavyo imeamua kufanya hivyo kwa wazee.